1 Chronicles 17:16-27

Maombi Ya Daudi

(2 Samweli 7:18-29)

16 aNdipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za Bwana, akasema:

“Mimi ni nani, Ee Bwana Mungu, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta mpaka hapa nilipo?
17Kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee Mungu, umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Umeniangalia kama mtu aliyetukuka kuliko watu wote, Ee Bwana Mungu.

18 b“Daudi aweza kukuambia nini zaidi kuhusu kumheshimu mtumishi wako? Kwa maana wewe unamjua mtumishi wako, 19 cEe Bwana Mungu. Kwa ajili ya mtumishi wako, tena sawasawa na mapenzi yako, umefanya jambo hili kubwa sana na kujulisha ahadi hizi zote zilizo kubwa sana.

20 d“Hakuna aliye kama wewe, Ee Bwana Mungu, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe. 21 eNaye ni nani aliye kama watu wako Israeli: taifa pekee duniani ambalo Mungu wake alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe na kujifanyia jina kwa ajili yake mwenyewe, kwa kufanya maajabu makubwa na ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri? 22 fUliwafanya watu wako Israeli kuwa watu wako wewe mwenyewe milele, nawe, Ee Bwana Mungu, umekuwa Mungu wao.

23 g“Sasa basi, Bwana ahadi uliyoweka kuhusu mtumishi wako na nyumba yake na uithibitishe milele. Fanya kama ulivyoahidi, 24 hili ithibitike na jina lako litakuwa kuu milele. Kisha watu watasema, ‘Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu aliye juu ya Israeli, ndiye Mungu wa Israeli.’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itafanywa imara mbele zako.

25“Wewe, Mungu wangu, umemfunulia mtumishi wako Daudi kwamba utamjengea yeye nyumba. Hivyo mtumishi wako amekuwa na ujasiri wa kukuomba maombi haya. 26 iEe Bwana, wewe ndiwe Mungu! Umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri. 27 jBasi imekupendeza kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu milele machoni pako; kwa ajili yako, Ee Bwana, umeibariki, nayo itabarikiwa milele.”

Copyright information for SwhNEN